Loading trending stories…
Kanisa Katoliki litakavyowaombea waliothiriwa na vurugu za Oktoba 29
Back to Home

Kanisa Katoliki litakavyowaombea waliothiriwa na vurugu za Oktoba 29

Mwananchi 31 minutes 3 mins read
Dar es Salaam. Mwaka mmoja baada ya matukio ya yaliyoambatana na Uchaguzi Mkuu wa 2025, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limezitaka parokia, vituo vya sala na taasisi za Kanisa Katoliki nchini kuadhimisha misa takatifu maalumu ya kuwaombea watu waliouawa, waliopotea, waliojeruhiwa na waathirika wengine wa matukio yaliyotokea wakati wa uchaguzi huo. Wito huo umetolewa na Rais wa TEC, Askofu Wolfgang Pisa kwenda kwa kardinali, maaskofu wakuu na maaskofu wote, kupitia barua ya kichungaji iliyowaelekeza kuadhimisha misa hizo zitakazofanyika Alhamisi, Oktoba 29, 2026. Hii si mara ya kwanza kwa TEC kutoa wito wa kuliombea Taifa na waathirika, wakiwemo waliouawa katika vurugu hizo. Novemba 15 ilitoa waraka mahsusi ikisema: “Tunawaombea pia uponyaji wa ndani wale wote walioathirika, kiroho, kisaikolojia na kiuchumi. Mwenyezi Mungu awape baraka na kitulizo. Mwisho, tunaendelea kuzikabidhi roho za marehemu wote waliouawa katika vurugu hizi wapate rehemu kwa Mungu na wapumzike kwa amani.” Katika kuwakumbuka waliopoteza maisha hata Chama cha ACT Wazalendo kupitia Ngome ya Wanawake, Machi 3, 2026 kilizindua mnara wa kumbukumbu na kuweka mashada ya maua kwa ajili hiyo. Si taasisi hizo tu zilizoona umuhimu wa kuwakumbuka watu hao, hata Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Ghasia na Uvunjifu wa Amani iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman ilipendekeza kuwepo siku maalumu ya kitaifa ya kuwakumbuka wote waliopata madhila kutokana na matukio hayo. Akiwasilisha ripoti yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan Aprili 23, 2026 Jaji Chande alisema: “Serikali itenge siku ya Maombolezo ya Kitaifa kuwakumbuka Watanzania zaidi ya 500 waliofariki kwenye ghasia za wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025”. Kwa mujibu wa ripoti hiyo watu 518 walipoteza maisha na wengine 2,390 walijeruhiwa. Hata hivyo, hadi sasa Serikali haijatangaza hatua zozote za utekelezaji wa pendekezo hilo. Kwa sasa inaendelea na utekelezaji wa pendekezo la kuunda Tume ya Uchunguzi wa Kijinai ambayo ilishaundwa chini ya uenyekiti wa Jaji Shabani Lila inayoendelea kukusanya maoni. Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema kwa sasa uamuzi huo haujafikiwa lakini kumekuwepo na majadiliano kuhusu pendekezo hilo. Amesema upo upande unaosema si muhimu kwa sababu itatonesha vidonda kwa waathirika, wapo wanaotaka ifanyike. Katika mazingira hayo, bado Serikali haijafanya uamuzi. “Ni kweli Tume ilipendekeza, lakini si kila pendekezo linatekelezwa haraka, yapo yanayohitaji tathmini ya kina," amesema. Waraka wa TEC Katika waraka wa TEC ulioandikwa Oktoba 23, 2026, Askofu Pisa amesema Kanisa linaona ni muhimu kuendelea kuliombea Taifa pamoja na wale ambao bado wanaishi na maumivu yaliyosababishwa na matukio ya uchaguzi wa mwaka jana. “Aidha, tunakumbuka baadhi ya watu wetu kuumizwa, kupotea na hata kuuawa. Hali hiyo ya maumivu na msiba bado ipo kati ya watu wetu,” amesema askofu Pisa kwenye waraka huo. Amesema katika kipindi hicho cha kumbukizi, “Katika mazingira haya tunaitwa kusimama pamoja kama jumuiya ya waamini, tukimkabidhi Mwenyezi Mungu mwenye huruma, Taifa letu, viongozi na watu wake. Tukiomba umoja, upendo, ukweli na mshikamano, ambavyo ni matunda ya haki na amani.” Kwa mujibu wa TEC, misa hizo zinaweza kuadhimishwa katika muda wa kawaida wa asubuhi au wakati mwingine unaofaa kulingana na utaratibu wa kila parokia, huku masomo ya siku au masomo maalumu yakiruhusiwa kutumika. Katika maelekezo hayo, Askofu Pisa amewataka waumini kuomba faraja kwa wanaolia, tumaini kwa waliokata tamaa, haki na ukweli kwa waliopotea, uponyaji kwa waliojeruhiwa na huruma ya Mungu kwa waliotangulia mbele zake. “Kwa sauti ya upole, unyenyekevu, unyofu na majuto tuombe faraja kwa wanaolia, tumaini kwa waliokata tamaa, imani kwa wenye mahangaiko, haki na ukweli kwa waliopotea, busara kwa wasioelewa, uponyaji kwa wenye majeraha na upendo kwa wenye chuki,” amesema.

This article was sourced from an external publication.

Share this article
OneClick Africa Logo

Africa's premier digital hub for impactful news, entertainment, and business insights.

© 2026 OneClick Africa. All rights reserved.