Loading trending stories…
Mv New Mwanza yaleta matumaini Afrika Mashariki
Back to Home

Mv New Mwanza yaleta matumaini Afrika Mashariki

Mwananchi 10 minutes 3 mins read
Kisumu. Mradi wa meli ya kisasa ya Mv New Mwanza umepongezwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ukitajwa kuwa fursa ya kuimarisha usafiri na ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi zinazozunguka Ziwa Victoria. Pongezi hizo zimetolewa katika Mkutano wa 24 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC), uliofanyika jijini Kisumu, Kenya, Oktoba 23, 2026. Meli hiyo, ilizinduliwa na Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba Januari 23, 2026 katika Bandari ya Mwanza Kusini kwa safari ndani ya nchi kati ya Bukoba (Kagera) na Mwanza. Meli hiyo ilijengwa na mkandarasi kutoka Korea, Gas Entec Ship-Building, kwa kushirikiana na Kampuni ya Meli Tanzania (Tashiko) kwa gharama ya Sh120.56 bilioni. Ina uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo na magari 20. Mwenyekiti wa mkutano huo, Waziri wa Maji na Mazingira wa Uganda, Meja Jenerali mstaafu Kahinda Otafire, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuwekeza katika mradi huo, akieleza umuhimu wake kwa usafiri katika ukanda wa Ziwa Victoria. Fursa za meli Akizungumza baada ya mkutano huo, Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Reuben Kwagilwa alisema mradi huo una fursa za kuwahudumia wananchi wa ndani na katika nchi zinazopakana na Ziwa Victoria. Alisema Tanzania inatambua umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika kuhakikisha meli hiyo inanufaisha nchi wanachama na kurahisisha usafiri kati ya maeneo mbalimbali ya ziwa. Kabla ya mkutano huo, ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Charles Kadonya, ulitembelea Bandari ya Kisumu. Kadonya aliishukuru Serikali ya Kenya kwa ushirikiano inaoutoa katika kuwezesha meli hiyo kuanza kuhudumu katika Bandari ya Kisumu. Alisisitiza umuhimu wa nchi wanachama wa EAC kushirikiana kuhakikisha Ziwa Victoria linatumika kwa namna inayochochea maendeleo endelevu na kuleta manufaa kwa nchi zote zinazolizunguka, huku mazingira yake yakilindwa. Kadonya alisema Tanzania inalenga kuhakikisha meli hiyo inafika katika nchi wanachama ili kurahisisha usafiri wa wananchi kutoka eneo moja kwenda jingine. “Katika mkutano huu tumesikia wajumbe kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamepokea vizuri mradi huu wa meli na tunahakikisha meli hii inafika nchi zote wanachama, ili waweze kusafiri kwa urahisi kutoka eneo moja kwenda lingine, hatua hii ni mafanikio makubwa,” alisema. Katika mkutano huo, pia ulizinduliwa mpango mkakati wa kuimarisha usimamizi, utunzaji na hifadhi endelevu ya mazingira ya Ziwa Victoria. Mpango huo unaendana na ajenda ya nchi wanachama ya kuhakikisha rasilimali za ziwa hilo zinatumika kwa manufaa ya sasa bila kuhatarisha upatikanaji wake kwa vizazi vijavyo. Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria inajumuisha Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Somalia. Ushirikiano wa nchi hizo ni muhimu katika kusimamia rasilimali za ziwa na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika ukanda huo.

This article was sourced from an external publication.

Share this article
OneClick Africa Logo

Africa's premier digital hub for impactful news, entertainment, and business insights.

© 2026 OneClick Africa. All rights reserved.