Loading trending stories…
Rais Samia akutana na balozi wa Afrika Kusini, mwekezaji wa Qatar
Back to Home

Rais Samia akutana na balozi wa Afrika Kusini, mwekezaji wa Qatar

Mwananchi about 3 hours 3 mins read
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Afrika Kusini nchini, Noluthando Mayende-Malepe, anayemaliza muda wake wa utumishi, huku akijadiliana na mwekezaji kutoka Qatar kuhusu fursa za uwekezaji katika kilimo, ufugaji, uvuvi na miundombinu ya usafiri nchini. Mkuu huyo wa nchi, amekutana na wawili hao leo, Novemba 6, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam. Taarifa iliyotiwa saini na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu, imeeleza Rais Samia amempongeza Balozi Mayende-Malepe kwa mchango wake katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na Afrika Kusini. Balozi Mayende-Malepe, ambaye amehudumu nchini kwa miaka minne, amemshukuru Rais Samia, Serikali na wananchi wa Tanzania kwa ushirikiano na ukarimu alioupata katika kipindi chote cha utumishi wake. Amesema Tanzania imekuwa na nafasi ya kipekee katika maisha yake ya kidiplomasia kutokana na ukarimu wa Watanzania na uhusiano wa kihistoria na kindugu uliopo kati ya nchi hizo mbili. Uhusiano huo, amesema, ulijengwa tangu wakati wa harakati za ukombozi wa Bara la Afrika, ambapo Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi zilizochangia mapambano dhidi ya mifumo ya kikoloni na ubaguzi wa rangi. "Tanzania ndiyo nchi niliyoifurahia zaidi kuhudumu katika kazi yangu ya ubalozi," amesema Balozi Mayende-Malepe, akieleza kuwa anaondoka nchini akiwa na kumbukumbu nzuri za maisha na utumishi wake. Mbali na uhusiano wa kihistoria, Balozi huyo amepongeza mchango wa Tanzania katika masuala ya kikanda na kimataifa, huku akizihimiza kampuni za Tanzania kutumia fursa zilizopo kufanya biashara na kuwekeza Afrika Kusini. Kwa upande wake, Rais Samia amesema biashara kati ya Tanzania na Afrika Kusini imeongezeka katika kipindi cha miaka minne ya utumishi wa Balozi Mayende-Malepe. Hata hivyo, amesisitiza umuhimu wa nchi hizo kutumia fursa zilizopo kuongeza zaidi biashara na uwekezaji ili kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kunufaisha wananchi wa pande zote mbili. Balozi Mayende-Malepe aliwasilisha Hati ya Utambulisho kwa Rais Samia Agosti 25, 2022, na tangu wakati huo amekuwa akiwakilisha Serikali ya Afrika Kusini nchini Tanzania. Katika tukio jingine, Rais Samia amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa kampuni ya Thirty-Five Investment Holding ya Qatar, Dk Khalid bin Mohammed bin Abdullah Al Attiyah, kuhusu uwezekano wa kampuni hiyo kuwekeza katika sekta mbalimbali za uchumi nchini. Dk Al Attiyah, ameeleza nia ya kampuni yake kuwekeza katika kilimo na ufugaji, akitaja fursa za uzalishaji wa sukari na ufugaji wa ng'ombe katika eneo la Kongwa, mkoani Dodoma. Katika sekta ya uvuvi, mazungumzo yamejikita katika uwezekano wa kuwekeza kwenye uvuvi wa bahari kuu, pamoja na ujenzi wa mitambo ya uchakataji na miundombinu ya kuhifadhi samaki katika Bandari ya Uvuvi Kilwa. Hatua hiyo inalenga kuchochea uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa sekta ya uvuvi, ikiwamo kuongeza uwezo wa kuchakata na kuhifadhi mazao ya baharini. Aidha, Dk Al Attiyah amesema kampuni yake inatathmini fursa za uwekezaji katika miundombinu ya usafiri Zanzibar. Amesema majadiliano kuhusu miradi inayopendekezwa tayari yameanza kati ya timu ya kampuni hiyo na wataalamu kutoka taasisi husika za Zanzibar. Akizungumza kuhusu mipango hiyo, Rais Samia amezitaka taasisi za Serikali zinazohusika kuendeleza mazungumzo na kampuni hiyo kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni zilizopo. “Hatua hiyo itasaidia kubaini miradi yenye fursa halisi za kutekelezeka na kuhakikisha uwekezaji unaopendekezwa unaleta manufaa kwa pande zote,” amesema.

This article was sourced from an external publication.

Share this article
OneClick Africa Logo

Africa's premier digital hub for impactful news, entertainment, and business insights.

© 2026 OneClick Africa. All rights reserved.